ahazi john
AHAZI
Friday, November 1, 2013
TAARIFA KWA UMMA KUHUSU MITIHANI NA UPANGAJI WA ALAMA kidato cha nne na sita
TAARIFA KWA UMMA KUHUSU MITIHANI NA UPANGAJI WA ALAMA
| Print |
JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
WIZARA YA ELIMU NA MAFUNZO YA UFUNDI
UPANGAJI WA VIWANGO VYA ALAMA, MATUMIZI YA ALAMA ENDELEVU YA MWANAFUNZI NA UFAULU
1. UTANGULIZI
Wizara imekusanya maoni ya Wadau wa Elimu kuhusu Upangaji wa Viwango vya Alama (Grade Ranges)
katika Mitihani ya Kuhitimu Kidato cha Nne na cha Sita pamoja na Matumizi ya Alama za Tathmini
Endelevu ya Mwanafunzi (Continuous Assessment ama CA) kwa ajili ya kuamua kiwango cha ufaulu wa
mwanafunzi. Maoni ya wadau yamekusanywa kwa sababu kwa muda mrefu sasa upangaji wa viwango vya
alama vinavyotumika na utaratibu wake katika mitihani ya kuhitimu Kidato cha Nne na Kidato cha Sita
umekuwa haufanani pamoja na kwamba mitihani hiyo yote ni ya elimu ya sekondari. Pia mfumo masuala
mbalimbali ya mitihani katika elimu ya sekondari umekuwa na miundo tofauti ikiwemo ule unaotumika
shuleni na ule wa Baraza la Mitihani la Taifa. Kwa sasa kuna miundo mikuu miwili katika mfumo huo.
Muundo wa Kwanza ni upangaji wa viwango katika ngazi ya Shule ambapo Alama Mgando (Fixed Grade
Ranges) zifuatazo hutumika kupanga madaraja: A = 81 – 100; B = 61 – 80; C = 41 – 60; D = 21 – 40 na F = 0
– 20. Muundo huu umetumika kwa muda mrefu na umezoeleka kwa walimu na wanafunzi wa elimu ya
sekondari kwa ujumla.
Muundo wa Pili ni wa viwango vinavyotumiwa na Baraza la Mitihani la Taifa ambapo ambapo kabla ya
mwaka 2012 muundo wa viwango nyumbufu (flexible grade ranges) ulitumika. Katika muundo huu uwigo
wa alama ulibadilika badilika kulingana na hali ya matokeo ilivyokuwa kwa mwaka husika. Lakini kuanzia
mwaka 2012, Serikali iliamua kutumia mfumo wa Upangaji wa Alama Mgando (Fixed Grade Range) kwa
Kidato cha Nne na Kidato cha Sita. Katika mtihani wa Kidato cha Nne mwaka 2012 Baraza lilitumia mfumo
huu wa alama mgando ambapo: A = 80 – 100, B = 65 – 79, C = 50 – 64, D = 35 – 49, F = 0 – 34. Kwa
upande wa Kidato cha Sita Baraza lilitumia mfumo wa A = 80 – 100; B = 75 - 79; C = 65 – 74; D = 55 – 64; E
= 45 – 54; S = 40 – 44 na F = 0 – 39. Mifumo hii ya Baraza haikuwa inafahamika kwa wadau na hivyo kuwa
sehemu ya malalamiko katika sekta ya elimu na mafunzo.
Vilevile, Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 1995 imeelekeza kwamba katika kuamua kiwango cha
ufaulu wa mwanafunzi wa elimu ya sekondari, Alama za CA zitachangia asilimia hamsini (50%) na Mtihani
wa mwisho utachangia asilimia hamsini (50%). Kwa upande wa Zanzibar, CA zimekuwa zikiandaliwa kwa
mfumo wa asilimia arobaini (40%) na mtihani wa mwisho asilimia sitini (60%). Pamoja na kwamba Baraza
halijawahi kuutumia mifumo hii tangu ilipowekwa, kumekuwa na mitazamo, maoni na mapendekezo
tofauti katika muundo na matumizi ya alama za CA. Kuna mawazo pia kwamba mfumo wa CA kuchangia
matokeo ya mwisho ya mwanafunzi pia utumike kwa watahiniwa wa kujitegemea (private candidates).
Kwa sasa matokeo ya mitihani ya watahiniwa hawa yamekuwa yakitumia alama za mtihani wa mwisho tu
na hivyo kutafsiriwa kama utaratibu ambao unamwonea mwanafunzi ambaye anahamu ya kujiendeleza
kielimu lakini anakwama kwa sababu mfumo unaotumika siyo rafiki kwa mtahiniwa.
Kwa mantiki hii, Wizara imedhamiria kufanya harmonization ya masuala ya alama katika mitihani ya
Kidato cha Nne na Kidato cha Sita ili kupata muundo mmoja na ulio wazi kwa wadau wote wa elimu ya
sekondari. Lakini pia serikali imedhamiria kuhakikisha tathmini za wanafunzi katika ngazi mbalimbali
zinakwenda sambamba na matarajio ya mitaala inayotumika na ambayo inahuishwa mara kwa mara ili
iendane na wakati na mahitaji ya elimu katika ngazi mbalimbali.
2
2. DHANA YA MITIHANI NA ALAMA
Mitihani hutumika kwa madhumuni mbalimbali ikiwemo kupima endapo malengo ya kujifunza na
kufundisha yamefikiwa na pia kubaini changamoto mbalimbali katika utoaji wa elimu katika ngazi husika.
Kimsingi, mfumo wa mitihani ni jambo linalopangwa kwa kuangalia mambo mbalimbali ikiwemo hali halisi
ya elimu katika ngazi husika. Mfumo unaweza kubadilika kulingana na elimu inavyoendelea kukua na
mahitaji mbalimbali yanavyoendelea kujitokeza. Mtihani wowote lazima uwe na matokeo. Ili matokeo
haya yapatikane, kila nchi imejiwekea utaratibu wa kuyapata matokeo hayo kulingana na malengo
(objectives) ya mtihani husika.
Kitaalamu, mtihani una uhusiano mkubwa sana na mitaala (curricula) na mihtasari yake na jinsi mitaala
hiyo inavyofundishwa na wanafunzi kujifunza (curricula instruction or delivery). Mitihani pia huwa
inafanyika katika muda maalum na kwa hivyo kuna:
a) mitihani kwa ajili ya kupanga wanafunzi katika makundi (streams) kulingana na umahiri
wao (placement assessment),
b) mitihani ya kubaini kama ufundishaji unakwenda vizuri na changamoto zilizopo ili
kuchukua hatua rekebu kadri mwanafunzi anavyoendelea kukua kielimu (diagnostic
assessment),
c) mitihani ya kubaini ukuaji wa mwanafunzi kielimu (formative assessment) na
d) mitihani ya kumaliza elimu katika ngazi husika (summative assessment).
Mara nyingi mitihani ya kundi (a) mpaka (c) inaunda kundi la CA wakati ile ya kundi (d) inaunda kundi la
mtihani wa mwisho (final examination ama FE).
Ili upimaji ufanyike, ni lazima mtihani uwe na muundo stahiki wa alama (grading structure). Muundo huu
hupangwa kulingana na maamuzi ya uwigo gani utumike. Kwa mfano, ngazi nyingi za elimu hutumia
uwigo wa alama 0 hadi 100 na kuna sehemu nyingine uwigo wake ni 0 hadi 50. Kwa miaka mingi, uwigo
wa alama kwa Kidato cha Kwanza hadi cha Sita hapa nchini umekuwa wa alama 0 hadi 100.
Pia, kimsingi, kuna mifumo miwili ya upangaji wa viwango vya ufaulu duniani katika kutunuku ufaulu.
Baadhi ya nchi au mifumo hutumia viwango vinavyobadilika (flexible grade ranges) ambavyo hupangwa
kwa kutegemeana na ufaulu wa watahiniwa katika somo husika. Nchi au mifumo mingine hutumia
viwango visivyobadilika (fixed grade ranges) ambavyo hupangwa na nchi au mifumo husika vitumike kama
kipimo cha ufaulu kwa masomo mbalimbali.
Katika mitihani ya elimu ya sekondari, Tanzania ilifuata mfumo wa kutumia viwango vinavyobadilika
(Flexible Grades) kuanzia mwaka 1973 hadi 2011. Hata hivyo, kwa madhumuni ya kuwawezesha wadau
kujua viwango vya ufaulu vinavyotumika katika kutunuku matokeo ya mitihani ya taifa ya sekondari,
Serikali iliamua kuanza kutumika kwa utaratibu wa viwango vya ufaulu visivyobadilika (Fixed Grades)
kuanzia mwaka 2012. Suala kubwa lililokuwa limebaki lilikuwa ushirikishwaji wa wadau ili kuliweka wazi
suala hili na kila mdau aweze kujua mfumo na miundo yake ikiwemo mfiko wa alama na maana yake
katika kila kundi la alama.
3. MAONI YA WADAU
Kabla ya kuwashirikisha wadau, Wizara iliunda Kamati ndogo kupitia taarifa mbalimbali na kutoa
mapendekezo ya jinsi muundo wa alama katika mitihani ya Kidato cha Nne na Kidato cha Sita unavyoweza
kuwa. Kamati hii ilifanya kazi hiyo na kutoa mapendekezo yake ambayo nayo yalipelekwa kwa wadau kwa
ajili ya majadiliano zaidi. Wadau mbalimbali walishirikishwa katika kutoa maoni juu ya utaratibu mpya wa
upangaji wa viwango vya alama na ufaulu. Wadau hao ni pamoja na jukwaa la taasisi za elimu ya juu,
chama cha wakuu wa shule za Sekondari nchini (TAHOSSA) wakuu wa vyuo vya ualimu vya umma,
wamiliki na wakuu wa shule na vyuo visivyo vya Serikali (TAMONGSCO), wakaguzi wa shule kanda,
muungano wa wanafunzi wa Taasisi za elimu ya juu nchini (TAHLISO), viongozi wa Wizara ya Elimu na
3
Mafunzo ya Amali Zanzibar, walimu, wanafunzi, wazazi, maafisa elimu Mkoa, Wilaya pamoja na maafisa
taaluma wao, wadau kutoka Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Wanataaluma na Wanasiasa.
Maoni hayo yalikusanywa kupitia mikutano mbalimbali na kwa njia ya madodoso. Wadau wote
walikubaliana kwamba mfumo nyumbufu wa alama siyo mzuri na hivyo taifa lihamie kwenye mfumo wa
alama mgando katika mitihani mbalimbali.
Kwa jumla wadau walipendelea utaratibu wa upangaji makundi ya alama kwa kuzingatia muachano wa
alama kumi kumi kutoka kundi moja hadi jingine. Hali hii inasaidia kuondokana na muundo ambao
unawalundika wanafunzi wengi na mara nyingi wasiofanana katika uwezo wao kielimu katika kundi moja.
Aidha wadau walipendekeza kiwango cha chini cha ufaulu mzuri kuwa Cna hii iwe sawa na alama 40.
Kwa upande wa alama endelevu, wadau pia walipendelea kuwa CA ichangie asilimia 40 katika matokeo ya
mitihani ya kuhitimu ngazi husika ya masomo. Hata hivyo, wadau walitoa angalizo kwamba ni vyema
kukawa na muundo na utaratibu mzuri wa kuzipata alama endelevu za mwanafunzi. Muundo na utaratibu
huo unaweza kutumia mitihani ya Kidato cha Pili na ile ya mock ya Kidato cha Nne ambayo huwa
inaandaliwa, kusimamiwa na kusahihishwa kwa umakini na weledi wa kutosha. Pia mwalimu naye
asinyimwe fursa ya kuchangia kwenye alama za maendeleo ya mwanafunzi na hivyo matokeo ya mitihani
ya muhula wa kwanza na wa pili ya Kidato cha Tatu nayo yanaweza kutumika kama sehemu ya alama
endelevu. Hatua kali zichukuliwe kwa mtu na taasisi yoyote itakayobainika kukiuka maadili katika
usimamiaji na uwasilishaji wa matokeo ya mitihani.
Ili kuwaimarisha wanafunzi katika tasnia ya kufikiri na kuandika, kila mwanafunzi afanye project na
matokeo yake yatumike kwenye alama endelevu. Projects hizi zianze kuandaliwa wakati mwanafunzi
akiwa Kidato cha Tatu na kukamilishwa katika muhula wa kwanza Kidato cha Nne.
Kuhusu muundo wa madaraja, wadau wengi walishauri muundo uliopo sasa wa madaraja uimarishwe ili
kuanza kutumia muundo wa wastani wa alama katika ufaulu (Grade Point Average ama GPA). Muundo
huu huwa ni rahisi kueleweka na kuuandaa kuliko muundo wa madaraja. Lakini pia, kwa kutumia muundo
wa GPA inakuwa rahisi katika kukadiria uwezo wa mwanafunzi kielimu na kufanya maamuzi mbalimbali
ikiwemo kuendelea na masomo katika ngazi mbalimbali za elimu.
Mwisho, wadau walikubalianana pendekezo la muundo wa alama lijaribiwe katika mfumo halisi (actual
testing) ili kujua faida na athari zake katika mfumo wa elimu kama pendekezo hilo likitekelezwa. Matokeo
ya Kidato cha Nne mwaka 2012 na Kidato cha Sita mwaka 2013 yatumike katika kufanya majaribio na
hivyo wataalamu wa mifumo wa NECTA wafanye kazi hiyo na kuleta mapendekezo yao kabla ya uamuzi
wa mwisho kufikiwa. Hili lilifanyika (angalia Kiambatansho A Jedwali la 3 na la 4).
Baada ya majumuisho ya uchambuzi wa maoni ya wadau, Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi , Wizara
ya Elimu na Mafunzo ya Amali na Ofisi ya Waziri Mkuu -TAMISEMI walikutana na kushauriana nini
kifanyike katika kupanga viwango vya alama za mitihani na ufaulu. Katika kikao hicho, Mawaziri,
Makatibu Wakuu wa Wizara hizo na Kamishna wa Elimu, walipata nafasi ya kupitia maoni ya wadau,
kujadili na kupendekeza viwango vipya vya alama za ufaulu vitakavyotumika katika mitihani ya Kidato cha
Nne ya mwaka 2013 na Kidato cha Sita ya mwaka 2014. Viwango vilivyopendekezwa vilizingatia pia maoni
yaliyotolewa na wadau hapo juu na hivyo kuridhia kwamba Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi sasa
itangaze utaratibu wa alama za mitihani ya taifa kwa Kidato cha Nne mwaka 2013 na Kidato cha Sita
kuanzia mwaka 2014.
4. VIWANGO NA UTARATIBU KUANZIA MWAKA 2013 KWA KIDATO CHA NNE NA MWAKA 2014
KIDATO CHA SITA
Baada ya kufanya tathmini ya maoni mbalimbali ya wadau, misingi ifuatayo ilizingatiwa katika maamuzi
kuhusu makundi ya alama na muachano wake:
4
a) Alama zitakazotumika zitakuwa A, B, C, D, E na F. Muachano wa alama kati ya kundi moja hadi
jingine utafanana, isipokuwa tu pale ambapo itaonekana kuna sababu na hakuna athari za kuwa
na muachano tofauti na ule ambao umetumika katika makundi mengine.
b) Makundi ya alama hayatakuwa na clusters isipokuwa pale ambapo itaonekana kufanya hivyo
kunaleta tija katika kupata picha ya wahitimu kwa ajili ya matumizi mbalimbali. Kwa mantiki hii
(i) makundi ya alama A, C, D, E na F yabaki na cluster moja moja bali kundi la alama B
litakuwa na clusters mbili. Kundi la kwanza litakuwa la wale ambao wamepata alama kati
ya 50 mpaka 59 na litaitwa B na lingine litakuwa la wale ambao wamevuka uwigo wa 50
hadi 59 na kuelekea uwigo wa 60 hadi 74 na hili litaitwa B+ (angalia jedwali hapo chini).
(ii) Pamoja na kuwa na muachano wa alama 26 kama jedwali linavyoonesha hapo chini,
alama A kwa miaka mingi imekuwa ikianzia alama 75 hadi 100 na kwamba pamoja na
uwigo huo bado wanaofaulu kwa kiwango hicho ni wachache sana. Kwa mantiki hii,
hakuna haja ya kubadilisha uwigo ila juhudi ziendelee katika ufundishaji na ujifunzaji ili
kiwango cha ufaulu kiongezeke na kupata wanafunzi wengi zaidi wanaofaulu katika kundi
hili.
(iii) Pia, pamoja na kuwa na muachano wa alama 20 kama jedwali linavyoonesha hapo chini
kwa miaka mingi, huko shuleni mwanafunzi aliyepata alama 21 na hadi 30 alihesabiwa
kuwa na ufaulu wa chini kabisa au hafifu kwa kiwango cha alama D na ingawa ilikubalika
ufaulu wa aina hiyo kwa mazingira ya nchi yetu unaridhisha. Alama F ilikuwa ni kwa wale
waliopata chini ya hapo. Hivyo, alama F itaendelea kuwepo na itaanzia alama 0 hadi 19 na
E itaanzia alama 20 hadi 29 na D – 30 -39. Lengo la muundo huu ni kuwa alama
mbalimbali, isipokuwa kwa makundi machache, zianzie kwenye 0 yaani 0, 10, 20, 30, 40
na kuendelea badala ya kuanzia kwenye moja yaani 1, 11, 21, 31, 41 na kuendelea. Hii ni
kwa ajili ya kuleta mtizamo unaofanana katika ngazi mbalimbali za elimu ambapo kwa
sasa ngazi ambazo siyo za elimu msingi na sekondari zinatumia muundo wa kuanzia
kwenye 0 badala ya 1.
c) Uwigo wa jumla wa alama kwa Kidato cha Nne na Kidato cha Sita utaendelea kuwa wa alama 0
hadi 100 na kila kundi katika uwigo huu limepewa tafsiri kwa ajili ya kuamua mambo mbalimbali
yanayohusu maendeleo ya mwanafunzi kulingana na malengo ya mtihani husika. Kimsingi, tafsiri
zifuatazo zitakatumika
(i) Alama A itakuwa na maana ya ufaulu uliojipambanua (distincion or outstanding
performance),
(ii) Alama B+ itakuwa na maana ya ufaulu bora sana (excellent performance),
(iii) Alama B itakuwa na maana ya ufaulu mzuri sana ( very good perfomance),
(iv) Alama C itakuwa na maana ya ufaulu mzuri (good performance);
(v) Alama D itakuwa na maana ya ufaulu wa wastani (low performance),
(vi) Alama E itakuwa na maana ya ufaulu hafifu (very low performance), na
(vii) Alama F itakuwa na maana ya ufaulu usioridhisha (unsatisfactory performance).
Wataalamu katika maeneo mbalimbali ya elimu na ulimwengu wa kazi, kwa kushirikiana na
Wizara, watatoa maana ya tafsiri hizi kiutendaji katika maeneo yao kulingana pia na mahitaji yao.
d) Alama C iwe ndiyo alama ya ufaulu mzuri ambao hauhitaji urekebu wa lazima, wakati alama D na
E ni alama za ufaulu unaohitaji urekebu kadri mwanafunzi atakavyokuwa anaendelea na masomo
ili kuthibitisha kama mlengwa anaweza na kulingana na mahitaji ya eneo husika (targeted
remediation). Alama F iwe alama ya eneo linalohitaji urekebu wa hali ya juu (intesive remediation)
ili mwanafunzi huyo aweze kumudu masomo kadri anavyoendelea kukua kielimu ama
atakapoingia katika ulimwengu wa kazi.
e) Makundi ya alama yatajumuisha CA kwa kiwango cha asilimia isiyozidi 40 na mtihani wa mwisho
kwa asilimia isiyozidi 60 kwa makundi yote ya watahiniwa ikiwemo wale wa kujitegemea (private
5
candidates). Hii ni kwa kuzingatia kwamba CA siyo vizuri izidi uwigo wa alama ya ufaulu mzuri
unapoanzia ambayo ni C au 40.
f) CA kwa upande wa Kidato cha Nne zitokane na mtihani wa Kidato cha Pili (alama 15), matokeo ya
Kidato cha Tatu (alama 5 kwa kila muhula, na hivyo jumla ya alama 10), mtihani wa Mock (alama
10) na kazi mradi au Projects (alama 5). Kwa upande wa Kidato cha Sita, CA iendelee kutokana na
muundo unaotumika sasa.
g) CA zitumike pia kwa watahiniwa wa kujitegemea. Kwa upande wa watahiniwa wa kujitegmea
ambao wanarudia Mitihani, CA zao zitumike zile zilizotumika kutoa matokeo yake ya mitihani ya
awali. Kwa watahiniwa wa kujitegemea waliopitia mfumo wa Qualifying Test (QT), matokeo ya QT
yatumike kama CA na mtihani wa mwisho uchangie alama 60.
h) Kwa vile alama endelevu kwa mwaka 2013 kwa wanafunzi wa Kidato cha Nne tayari
zimeshawasilishwa Baraza la Mitihani Tanzania, alama hizo zichangie asilimia 40 katika mtihani
wa Kidato cha Nne mwaka 2013.
i) Muundo wa wastani wa alama katika ufaulu (Grade Points Average ama GPA) utaandaliwa na
kuanza kutumika pale utakapokuwa tayari na wadau wataelimishwa kuhusu muundo huo ili
wapate kuufahamu na manufaa yake katika elimu ya sekondari.
j) Muundo huu mpya wa alama utatumika kwa mzunguko wa miaka minne kabla haujahuishwa tena
ili kuupa muda wa kutosha kuona aina ya changamoto zinazojitokeza na jinsi ya kuzishughulikia.
Aina hii ya muda itaruhusu vidato vinne vya elimu ya sekondari ya kawaida na nane ya elimu ya
sekondari ya juu kupimwa. Hata hivyo, uhusihaji wa masuala ya mitihani unaweza ukafanyika
iwapo matokeo ya uhuishaji wa mitaala kwa ujumla utahitaji pia eneo la mitihani liguswe na
kuhuishwa pia.
Kwa mantiki hii, viwango vya alama na ufaulu ni kama inavyooneshwa kwenye jedwali la 1 hapa chini:
Jedwali Na 1
MUUNDO WA ALAMA NA UFAULU
ALAMA UWIGO WA ALAMA IDADI YA ALAMA TAFSIRI
A 75 - 100 26 Ufauli Uliojipambanua
B+ 60 - 74 15 Ufaulu bora sana
B 50- 59 10 Ufaulu mzuri sana
C 40 - 49 10 Ufaulu mzuri
D 30 - 39 10 Ufaulu Hafifu
E 20 - 29 10 Ufaulu hafifu sana
F 0 - 19 20 Ufaulu usioridhisha
Kwa aina hii ya muundo wa alama, na kwa kuwa muundo wa GPA utaanza kuandaliwa na wadau
kuelimishwa kabla haujaanza kutumika, katika kipindi hiki mpaka wakati huo, muundo wa madaraja
utakuwa kama inavyooneshwa kwenye jedwali la 2 hapa chini.
Jedwali Na 2
MUUNDO WA MADARAJA
MUUNDO WA ZAMANI MUUNDO MPYA MAELEZO
POINTI DARAJA POINTI DARAJA
6
7-17 1 7-17 I Kundi la ufaulu uliojipambanua na bora
sana
18-21 II 18-24 II Kundi la ufaulu mzuri sana
22-25 III 25-31 III Kundi la ufaulu mzuri na wa wastani
26-33 IV 32-47 IV Kundi ufaulu hafifu
34-35 0 48-49 V Kundi la ufaulu usioridhisha
Wataalamu wa mifumo ya mitihani watalifanyia kazi zaidi jedwali hili la madaraja ili liweze kutumika kwa
ufanisi katika kipindi hiki cha mpito.
Kwa mantiki hii, Daraja Sifuri linafutwa na kuwekwa daraja litakalojulikana kama Daraja la Tano na ambalo
litakuwa ndilo la mwisho kabisa katika ufaulu.
5. HITIMISHO
Mabadiliko haya yamefanyika ili kuendelea kuimarisha mfumo wetu wa elimu na kuweka wazi taratibu
mbalimbali kwa ajili ya mitihani na masuala mengine. Yako mambo mengi mengine ambayo hayana budi
kuendelea kuimarishwa ikiwemo mfumo wa mitaala, walimu, mazingira ya kujifunzia na kufundishia
pamoja na vitabu na vifaa vingine muhimu katika elimu. Masuala haya yanaendelea kuangaliwa kupitia
mikakati mbalimbali ikiwemo mpango wa Matokeo Makubwa Sasa ama Big Results Now (BRN).
Ushirikiano wa wadau wote ili kuleta tija kwenye elimu ni muhimu sana na hivyo wizara itaendelea
kuwashirikisha wadau wote kwa kadri itakavyohitajika na wadau pia wanaombwa wasiache kuishirikisha
wizara pale watakapokuwa na jambo lolote ambalo linahitaji ushirikiano ili kwa pamoja tuweze kupata
mafanikio katika sekta ya elimu.
Imetolewa,
KATIBU MKUU
WIZARA YA ELIMU NA MAFUNZO YA UFUNDI
TAAR
Newer Posts
Older Posts
Home
Subscribe to:
Posts (Atom)